Thursday, November 19, 2015
HUYU HAPA WAZIRI MKUU ALIYETEULIWA NA RAIS JPM LEO.
Dar es Salaam.
Rais John Magufuli leo amewasilisha bungeni jina la Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano.
Spika wa Bunge, Job Ndugai alipokea barua iliyotoka kwa Rais Magufuli kupitia kwa watumishi wa chombo hicho cha kutunga sheria na baada ya kuifungua ndipo aliposoma ujumbe huo uliotaja jina la Majaliwa ambaye alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu.
Baada ya tangazo hilo ambalo lilipokelewa kwa shangwe na wabunge wengi, Spika Ndugai aliahirisha bunge kwa dakika arobaini na tano kuwapa nafasi wabunge kutafakari uteuzi huo kisha kumthibitisha bunge litakaporejea.
Waziri Mkuu huyo mteule alizaliwa Disemba 22, 1960 na kupata elimu katika Shule ya Msingi Mnacho kati ya mwaka 1970-1976 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Kigonsera kati ya mwaka 1977- 1980.
Mwaka 1991-1993 alijiunga na Chuo Cha Ualimu Mtwara. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1994 na kuhitimu mwaka 1998 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden kwa masomo ya juu.
Amehudumu katika nafasi mbalimbali tangu mwaka 1984 alipojiunga na utumishi wa umma kama mwalimu mkoani Lindi, Katibu wa Chama cha Waalimu Wilaya, Katibu chama waalimu Mkoa na Mkuu wa Wilaya.
Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kabla ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kumteua mwaka 2012 kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu.
Subscribe to:
Posts (Atom)