Sunday, March 23, 2014

ARSENAL WAADHIBIWA VIKALI NA CHELSEA..

-Ni katika mechi ya 1,000 kwa kocha Arsene Wenger

- Refa atoa kadi nyekundu kwa mchezaji asiyestahili

Arsenal wameonja kichapo kikali zaidi katika Ligi Kuu msimu huu, katika siku ambayo kocha wake, Arsene Wenger ametimiza mechi ya 1,000 na klabu hiyo.
Washika Bunduki wa London walionekana kuanzia mguu mbaya tangu mwanzo, waliporuhusu mabao mawili ya haraka kupitia kwa Samuel Eto’o na Andre Schurrle dakika ya tano na ya sita katika dimba la Stamford Bridge.
Alex Oxlade-Chamberlain alichupa dakika ya 17 na kupangua kwa vidole mpira uliokuwa ukikaribia lango kwa juu kana kwamba ndiye alikuwa kipa, lakini mwamuzi Andre Marriner akakosea na kumpa kadi nyekundu Kierran Gibbs.
Marine alishikilia msimamo huo licha ya Oxlade-Chamberlain kumweleza kwamba ndiye aliyeunawa mpira huku Gibbs pia akieleza hakuwa ameshika mpira huo. Wachezaji wa Arsenal pia walielekea kupinga lakini mwamuzi hakubadilisha uamuzi wake.
Kwa mpira kushikwa na mchezaji ndani ya eneo la penati, ilitolewa adhabu hiyo na Eden Hazard hakuwa na tabu yakuukwamisha mpira wavuni akimwacha kipa Wojciech Szczesny bila la kufanya na kuwa bao la tatu.
Kutolewa kwa Gibbs kulitoa mwanya kwa nahodha Thomas Vermaelen kuingia kwa gharama ya Mjerumani Lukas Podolski kwenda nje, na mafuriko yaliendelea kwa bao la dakika ya 42 la Oscar kasha wakaenda mapumziko.
Kipindi cha pili Arsenal hawakuweza kuuona mlango wa Chelsea, bali waliruhusu mabao mawili zaidi kupitia kwa Oscar katika dakika ya 66 na Mohamed Salah dakika ya 71. Huu ndio ushindi mkubwa zaidi wa Jose Mourinho ndani ya Chelsea na pia ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kuwafunga wenzao wa London kwa idadi kubwa hivyo ya mabao.
Wenger atataka kuisahau siku hii muhimu kwake, ambapo Chelsea walizidisha pengo la pointi dhidi ya Arsenal kutoka nne hadi saba. Bado Arsenal wana kibarua kizito dhidi ya Manchester City Jumamosi ijayo, lakini watacheza kwanza na Swansea Jumanne hii.
Wenger alijiunga na Arsenal 1996 na ndiye anayeongoza England kwa kudumu muda mrefu zaidi kwenye timu moja, baada ya kustaafu kwa Alex Ferguson wa Manchester United mwaka jana, baada ya kukaa hapo kwa miaka 26 na nusu.

No comments:

Post a Comment