Monday, June 2, 2014

TAIFA STARS WAREJEA VEMA TANZANIA BAADA YA USHINDI MZITO.

9s4a0125
Kikosi cha Taifa Stars ambacho jana (Juni 1 mwaka huu) kiliitupa Zimbabwe (Mighty Warriors) nje ya michuano ya Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 kinarejea nchini leo (Juni 2 mwaka huu) kutoka Harare.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam saa 12.30 jioni kwa ndege ya Kenya Airways ikitokea Harare kupitia Nairobi.
Stars imefuzu kucheza raundi inayofuata kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2, kwani awali (Mei 18 mwaka huu) iliifunga Zimbabwe bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika raundi ya pili, Taifa Stars itacheza na Msumbiji ambapo itaanzia nyumbani kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.
Wakati huo huo, Taifa Stars imeendelea kupokea salamu za pongezi kutoka kwa wadau mbalimbali baada ya kufanikiwa kuvuka kikwazo hicho cha kwanza katika harakati zake za kucheza Fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Salamu hizo zimetoka kwa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Manyara (MARFA), mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA), John Kadutu, na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ahmed Idd Mgoyi.

No comments:

Post a Comment